Skip to main content

Uendelezaji wa elimu ya kimataifa kupitia kwa mikusanyiko ya kimataifa

Imetafsiriwa na Florence Mugambi na Peter Mwangi

Black Dawn, 1979

Tangu 2013, Chuo Kikuu cha Northwestern kimeitambua wiki ya kuadhimisha elimu ya kimataifa kama wakati wa kuenzi ongezeko na uwakilishwaji wa wanafunzi wa kimataifa chuoni, hali kadhalika hazina adhimu inayotokana na uzoefu unaowatayarisha Wildcats kuwa raia wa kimataifa.

Mwaka huu, Maktaba za Northwestern zinaangazia mikusanyiko michache miongoni mwa mikusanyiko anuai inayoendeleza uwepo wa miingiliano ya tamaduni tofauti zinazokifanya chuo kuwa kitovu cha mitagusano katika kiwango cha kimataifa.

 

Maktaba ya Masomo ya Kiafrika ya Herskovits

Maktaba ya Masomo ya Kiafrika ya Melville J. Herskovits katika chuo kikuu cha Northwestern iliyoanzishwa mnamo 1954 ina mkusanyiko wa Kiafrika mkubwa zaidi mahali popote. Upeo wake ni mpana kama lilivyo bara la Afrika lenyewe; ina hazina katika nyanja mbalimbali kama vile sanaa, historia, fasihi, muziki, sayansi, teknolojia, mawasiliano,  uhandisi, umeneja/usimamizi na upishi. Huwahudumia maprofesa na wanafunzi wa Northwestern, na hali kadhalika zaidi ya wasomi wa kimataifa elfu moja kila mwaka.

Zaidi ya dhima yake inayotokana na  mkusanyiko wa hazina adhimu, ni kiungo muhimu cha washirika wa chuo katika kuielewa Afrika zaidi. Mifano ni pamoja na:

Histoire_HerskovitsHistoria ya mashirika ya wanafunzi nchini Ufaransa, 1900-1950,Amady Aly Dieng, 2011.
Chini ya taratibu za utawala wa koloni za Ufaransa, WaAfrika walikuwa na nafasi chache za kufikia elimu ya juu; lengo kuu lilikuwa la kuwatayarisha wafanyi kazi wasaidizi wa  umma. Kufikia mwisho wa Vita Vikuu II vya dunia nchini Ufaransa, idadi ya wanafunzi WaAfrika katika elimu ya juu iliongezeka kutokana na ongezeko la ufadhili. Kipindi cha 1945-1950 kilishuhudia uanzishwaji wa mashirika ya kisiasa na hali kadhalika ya wafanyikazi na wanafunzi wa kiafrika waliosoma nchini Ufaransa, ili kupigania uhuru.

Afrika katika Northwestern na Chicago
Maktaba ya Herskovits na Programu ya Masomo ya Kiafrika zimeshirikiana kutoa kiungo kimoja cha raslimali ambazo chuo cha Northwestern hutoa kwa wanafunzi kutoka Afrika, au wanaopanga kuzuru Afrika, au walio na hamu ya kujifunza zaidi. Vitengo ni pamoja na  programu, raslimali za kielimu na utafiti, mashirika ya sanaa, mashirika ya wanafunzi, na vyanzo vya ufadhili.

 

Majarida: Habari kutoka kote ulimwenguni

Hong Kong JournalMagazeti ni nyenzo mwafaka ya kujua kuhusu yanayoendelea katika ulimwengu tunamoishi, na maktaba zinayapata magazeti kutoka pembe zote za dunia ili kuwawezesha wanafunzi kufahamu yanayojiri. Mara kwa mara unajipata mbali na nyumbani na unahitaji kufahamu yanayoendelea nyumbani au unahitaji kujiliwaza kwa kusoma mambo unayoyafahamu. Au pengine unajitahidi kusafiri ng’ambo na unajifahamisha na unakotembelea, labda kinachoendelea huko, kuukuza ufasaha wako wa lugha. Hapa kuna baadhi ya viungo muhimu

Hazina ya Magazeti/Press Reader
Hazina hii (Press Reader) hukuwezesha kuyaafikia magazeti matajika kama Sayansi ya Uturuki, Romania Iliyotandazika, na GQ Afrika Kusini. Hazina hii hukuwezesha kuyapata magazeti na majarida ya hivi majuzi kutoka kwa nchi na lugha 100, yanayoonyeshwa jinsi yalivyochapishwa. Inakaribiana na gazeti au jarida halisi mikononi mwako.

Zipate Habari za Dunia/Access World News
Access World News inasheheni maelfu ya magazeti ya kimataifa ikiwa ni pamoja na habari za kina za kihistoria na hali kadhalika matukio ya sasa hivi. Unapotafuta habari kutoka mahali maalum, ni rahisi kuyatalii maeneo tofauti au nchi kwa kutumia kiungo cha ramani ambacho ni rahisi kutumia.

 

Masomo ya Kituruki

Mkusanyiko mzima katika maktaba huendeleza Programu ya Masomo ya Kituruki cha Kisasa ya Keyman katika Taasisi ya Masomo ya Kimataifa ya Roberta Buffett katika Chuo Kikuu cha Northwestern, ambayo hutoa nafasi za kulikuza jukwaa la mwingiliano wa masomo unaopelekea kuelewa, kuwekeza, na kusoma Kituruki cha kisasa. Programu hudhamini shindano la hela za utafiti wa Masomo ya Kituruki cha Kisasa kwa maprofesa, wanafunzi wa shahada zote na pia hutoa hela kwa wasomi wa kutoka Uturuki kufundisha na kufanya utafiti katika Northwestern.

Mifano ya mkusanyiko huu ni pamoja na:

Mitandao ya Kijamii na Siasa Nchini Uturuki: Safari Kupitia kwa Wanahabari Raia, Dhihaka za Kisiasa, na Habari Potoshi, Erkan Saka, 2020.
Saka huangazia vyombo vya habari katika mitazamo ya kihakiki na kinzani ya matumizi ya mtandao nchini Uturuki. Kitabu hiki kinajadili matumizi ya uanahabari wa kiraia na hali kadhalika kampeni za kupotosha. Kitabu hiki kinawantambua wanaharakati wa kidigitali na kuhoji kuwa uhamasishaji kupitia kwa mitandao ya kidigitali kunatoa mwanga wa matumaini katika kuzipa changamoto serikali za kiimla.

We Are Arrested#Tumekamatwa, Pippa Hill, 2019
Tamthilia yake Hill iliyochota kutoka kwa kumbukumbu za Can Dundar kuhusu kukamatwa kwake baada ya kuchapisha video za idara ya ujasusi ya taifa la Uturuki ikisafirisha silaha hadi Syria. Tamthilia ilikuzwa na Sophie Ivatts na Pippa Hill kutoka kwa kampuni ya Royal Shakespeare na kuwasilishwa London katika Ukumbi wa Maonyesho wa Arcola mnamo majira ya maanguko ya 2019. Uhakiki wa kazi hii uliochapishwa katika Financial Times ulisema, “Ni kazi ya dakika 75 yenye kuchochea hisia kali, iliyoelekezwa na Ivatts, inayoakisi upweke wa mtu mwenye msimamo imara katika nchi inayouchukulia ukweli kuwa usaliti.”

Ataturk kwenye Sinema: Sinema ya Matukio Halisi na Ufanyikaji wa Kiongozi, Enis Dinc, 2020
Hili ni somo kuhusu picha za sinema za Ataturk lililoundwa/tengenezwa punde tu baada ya Vita I vya Dunia. Uchambuzi mkuu katika kitabu ni kuhusu filamu yenyewe, hali kadhalika marejeleo ya sinema za kisasa ambazo hazijapata uchambuzi wa kina kabla. Kitabu pia kinatumia marejeleo ya kimsingi kama vile barua, arifa, magazeti, ripoti, majarida na faili, na hivyo kuwapa wasomaji hali ya wakati ule kama ilivyotokea.

 

Habari za Serikali ya Marekani

Mkusanyiko huu wa raslimali za umma unajumuisha mitazamo ya ulimwengu iliyotolewa kupitia mashirika ya serikali anuai (IGOs) kama vile Umoja wa Mataifa, Shirika la Uchumi, Ushirikiano & Maendeleo (OECD), Shirika la Afya Duniani, na mengine mengi. Wakutubi wanaweza kuwaelekeza watafiti kupata raslimali muhimu zinazotokana na mashirikia yanayofadhiliwa na serikali.

Kwa mfano, Programu ya Utahini wa Wanafunzi Kimataifa (PISA) ya OECD huwezesha ulinnganishi wa kimataifa wa mifumo ya elimu, jinsi wanafunzi wanavyosoma na uwezekano wa wanafunzi kufanikiwa katika mataifa mengi. Matokeo ya PISA hutumiwa katika kuchangia maendeleo katika nchi za mapato ya chini na wastani zenye nia ya kufanya mageuzi ya kielimu kukuza malengo ya maendeleo endelevu  (SDG) ya ubora na usawa wa matokeo/malengo ya  masomo ya watoto, vijana, watu, na watu wazima. PISA 2018 Juzuu la VI ndiyo ripoti ya hivi majuzi yenye kichwa, Wanafunzi wako tayari kufanikiwa katika ulimwengu uliotandazika?

Klabu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu inawalenga wasomaji wa kati ya miaka 6-12 ili kuwawezesha kujifunza kuhusu mradi wa Umoja wa Mataifa wa kukuza ustawi na wakati uo huo kuihifadhi dunia. Toleo la kila mwezi la kitabu huangazia mojawapo ya malengo anuai 17 kama vile vita dhidi ya umaskini, kuondoa janga la njaa, na kuzihifadhi haki za kibinadamu. Raslimali nyingine zilizomo hapa ni pamoja na blogu yenye maandishi kutoka kwa washirika wa vikundi vya vitabu, maelezo kuhusu jinsi ya kuanzisha vikundi vya vitabu, na nyinginezo. Makavazi ya matoleo ya orodha za kila mwezi za vitabu pia yanapatikana.

 

Maktaba ya Muziki

Mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya muziki Marekani, Maktaba ya Muziki ina uwezo usiofananishwa katika muziki wa karne ya ishirini na wa kisasa, na iko na kama nakala moja ya kila chapisho jipya lililochapishwa tangu mwaka wa 1945. Wakutubi wa muziki wanaweza kuwaongoza watu kwa rasilimali iwezeshayo utendaji, ihimizayo uumbuji wa kazi mpya za muziki, na kutuwezesha kuelewa mahali na umuhimu wa muziki maishani mwa watu na tamaduni za ulimwengu. Mifano miwili ni:

Smithsonian FolkwaysSauti ya Dunia ya Smithsonian
Shehena hii ya data yenye uwezo wa kutiririza sauti itakuletea muziki kutoka ulimwenguni kote kwenye masikio yako. Kwa kuwa imejengwa kwenye kusanyiko kuu lililorekodiwa la Smithsonian Folkways, watumiaji wake wanaweza kutafuta kwa misingi ya nchi, vitengo, na watu. Rekondi nyingi ni “rekondi za nyanjani”, zilizonaswa na wanaethnografia wa muziki walipowatafitia watu wa kale duniani. Rekondi nyingine nyingi zinatolewa kwa malengo ya kibiashara katika nchi husika. Pasipo kujali chanzo chake, kifaa hiki hutoa nafasi ya kutalii muziki kutoka ulimwenguni kote.

Ensaiklopidia ya Muziki wa Dunia ya Garland
Ni ensaiklopidia ya mtandaoni yenye majuzuu 10, ambapo watumiaji wake wanaweza kujifunza kuhusu muziki na tamaduni kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Kila juzuu hutalii bara zima, na mada huwa ni kutokea muziki mwepesi “maoenyesho” hadi “sanaa” changamano ya muziki uliotungwa na tamaduni tofauti. Kila kitengo huandikwa na mtaalamu mtajika wa aina ya muziki husika.

 

Maktaba ya Usafiri

Maktaba ya Usafiri ya Chuo Kikuu cha Northwestern ilianzishwa mnamo mwaka wa 1958 kusaidia programu za mitaala na utafiti katika Chuo Kikuu cha Northwestern Idara ya Usafiri na Idara ya Usalama wa Umma. Ikiwa na vitu zaidi ya 500,000, Maktaba hii ni moja ya zile maktaba kubwa sana za usafiri ulimwenguni, na inajumuisha habari zote za nyenzo za usafirishaji kama  hewa, reli, barabara, bomba la mafuta, maji, usafiri mjini, na vifaa. Mark Twain aliwahi kutoa kauli maarufu aliposema “usafiri ni hatari/mbaya kwa ubaguzi, ushabiki wenye misingi potovu, na mawazo finyu.” Hapa pana rasilimali nzuri kuhusu vile watu wamesafiri miaka mingi.

Ethiopian Airlines timetableKusanyiko la Ratiba la George M. Foster
MwanaAthropojia mwasisi na mwanafunzi mkongwe wa Northwestern George M. Foster alisafiri kwa ndege ya abiria kwa mara ya kwanza mnamo 1935. Katika miongo saba iliyofuata, alisafiri kwa ndege, gari moshi, na boti mara nyingi kwa kazi yake kama MwanaAthroporojia na kama mshauri kwa mashirika kama vile Shirika la Afya Duniani na UNICEF. Kusanyiko la George M. Foster ni la kimataifa kwa upeo na husheheni ratiba 1766, nyingi zake zikiwa ni za ndege lakini pia za treni, meli, na boti zilizotelewa baina ya 1929 na 1991.

Kusanyiko la William Luke la Usafirishaji
Kusanyiko la William Luke la Usafirishaji hujumuisha zaidi ya ramani za maeneo ya karibu ya  usafirishaji 6200, ratiba, tiketi za usafiri, kadi za posta na stakabadhi nyininge kutoka nchi 98 na majimbo 38 ya Marekani, zilizotolewa na mwanahistoria wa kampuni ya basi na mwanzilishi wa Jarida la Safari  ya Basi (Bus Ride Magazine), William Luke. Ramani na ratiba zilitolewa kwa lengo mahsusi la kutumiwa na watalii. Kusanyiko hili liko katika lugha 34 na tarehe zake ni kutoka 1935 hadi 2012.

 

Utiririkaji wa Habari na Filamu

Maktaba za Northwestern zina kusanyiko kubwa la vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na filamu za kimataifa, matoleo huru, na sinema fupi kuhusu matukio halisi (documentaries). Kwa bahati nzuri, wakati huu wa janga la kimataifa, shehena kubwa inaweza kutiririshwa bora mtu awe na Intaneti na kitambulisho cha Northwestern. Chache  unazoweza kutazama wikendi hii ni pamoja na:

Hedgehog's HomeNyumba ya Nungunungu: ni filamu ya dakika kumi  kuhusu heshima ya makazi ya hali ya chini inayotumia wanasesere iliyoelekezwa na Eva Cvijanovic’ kutoka Kanada. Inasimulia mojawapo wa kisa ambacho kimesomwa sana cha Mkejeli Msabia wa karne ya 20, Branko Copic. Copic alikuwa mwandishi mashuhuri  wa fasihi ya watoto na aliyepigwa marufuku na serikali ya Yugoslavia kwa kuihakiki jamii ya kikomunisti.

Alfajiri Nyeusi: inasimulia jinsi Haiti ilivyoasisiwa kupitia kwa  macho ya mateka wawili wa kabila la Kiafrika, Sili na Simba. Filamu hii ya 1979 imefanywa kwa kuihuisha michoro ya Wanasanaa 13 wa Haiti wakiwa ni pamoja na Rignaud Benoit, Philom Obin, na Philippe Auguste.